Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) nchini kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yenye fursa katika kilimo ili kuongeza mapato yao.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 05 Novemba, 2022 Moshi Mkoani Kilimanjaro aliposhiriki katika uzinduzi wa huduma za kimtandao na kadi ya ATM za ELCT ND SACCOS ambayo ni washirika wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini.

"Dunia ya leo ni ya utandawazi, ninawapongeza sana kwa ubunifu wenu wa kuja na huduma hizi ambazo zitarahisisha kuwafikia wanachama wenu pasipo kutakiwa kufika ofisini kwenu. Nawatia shime viongozi wote wa ELCT ND SACCOS kuzidi kutafuta maarifa ambayo yatakwenda kurahisisha huduma kwa wanachama wenu".

Mavunde alibainisha kuwa maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) tunasimamia maendeleo ya ushirika nchini, na ndiyo maana tumeweka msukumo mkubwa katika kuimarisha mifumo ya utendaji wa vyama vya ushirika zikiwemo SACCOS ili ziweze kujiendesha kwa tija na kuwa mwokozi kwa wanachama wao.

"Kupitia Ajenda 10/30 ambayo inalenga kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, tumejiwekea vipaumbele mbalimbali ikiwemo utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuimarisha huduma za ugani na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Tunazikaribisha SACCOS zote mkiwemo ninyi kuja kutuunga mkono katika kuendeleza kilimo nchini kwenye maeneo yenye fursa kubwa kama uzalishaji wa mazao ya mafuta, ngano na sukari," aliongeza Mhe. Mavunde.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde aliiagiza TCDC kupitia mfumo wao wa kidijitari wa kusajili vyama na wanachama wote wa ushirika nchini kuendelea kuusimamia na kuuboresha ili uende kuwa suluhuhisho ya baadhi ya changamoto za maendeleo ya ushirika Nchini.

Aidha, Mhe. Mavunde ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika vyote nchini kujitokeza kwa wingi kununua hisa za Benki ya Taifa Ushirika ambayo ipo katika hatua za mwisho kuanzishwa, ili kuiwezesha kimtaji na kuwa sehemu ya wamiliki wa benki hiyo.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Juma Igando aliipongeza SACCOS ya ELCT ND kwa mafanikio ya kuanza kwa mifumo hiyo na kueleza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili ushirika uweze kuwa na tija kubwa kwa wanachama wake.

Naye Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Collins Nyakunga alimshukuru Naibu Waziri wa Kilimo kwa ushiriki wake katika uzinduzi huo na kuahidi kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kukuza na kuimarisha sekta ya ushirika nchini.