Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kupata leseni kabla ya tarehe 30 Aprili, 2024 ili SACCOS hizo kuleta tija kwa wanaushirika na taifa kwa ujumla.

Gavana ametoa wito huo leo tarehe 22 Septemba, 2023 wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo ( SACCOS) kwa mwaka 2022 iliyofanyika Jijini Mwanza.

"Napenda kuwakumbusha kwamba muda wa mpito wa kupata leseni hizo uliotolewa na Benki Kuu unakaribia kuisha, muda huo utaisha mnamo tarehe 30 Aprili 2024. Hivyo, ni vema SACCOS hizo zikatumia muda huu uliobaki," amesema Gavana

Aidha, Gavana ametoa wito kwa SACCOS zote Tanzania Bara kuendelea kuupa nguvu muungano wao ili uweze kuwahudumia vema wanachama.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife akiongea Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika amesema kuwa Tume itaendelea kushirikiana na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo SACCOS ili kufikia malengo ya kukua kiuchumi.

Akiwasilisha Taarifa ya Utendaji wa SACCOS, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt.Benson Ndiege amesema kuwa SACCOS zinatakiwa kusajiliwa kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Ushirika kabla ya kuomba na kupewa leseni za kutoa Huduma Ndogo za fedha.

"Chama kikisajiliwa kinakuwa na sifa za kuomba na kupewa leseni ya huduma ndogo za Fedha kwa mujibu wa sheria ya huduma ndogo za fedha na Kanuni zake."