Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, ametoa wito kwa Wananchi kutumia Huduma rasmi za Kifedha zilizosajiliwa na zenye kutambuliwa ili kuepuka usumbufu unaotokana na huduma za Mikopo yenye kuumiza Wananchi kiuchumi.
Hayo yamesemwa Jijini Mbeya Septemba 5, 2024 wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa mwaka 2023 iliyoandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Amesema, huduma jumuishi za kifedha kwa Watanzania ni sehemu ya malengo ya Serikali ambapo Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau, wamekuwa wakisimamia.
“Naomba nitoe wito kwa SACCOS kuendelea kufungua milango zaidi kwa wananchi, na kwenda maeneo mbalimbali ambayo huduma za kifedha bado hazijafika vizuri ili kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanafikiwa na mifumo rasmi ya huduma za kifedha,” amesema.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, akiwasilisha Taarifa hiyo amebainisha kuwa miongoni mwa malengo ya Taarifa hiyo ni kuweka uwazi na taarifa juu ya utendaji wa SACCOS nchini kwa mwaka husika na kujua maeneo yenye changamoto ili kuboresha zaidi.
Ameongeza kuwa kwa mwaka 2023 SACCOS zilizoomba Leseni ni 1,215, zilizopata Leseni ni 884 na zilizokosa Leseni ni 331.
Akibainisha kuwa idadi hiyo inadhihirisha kuwa uelewa wa uendeshaji wa SACCOS umeongezeka na kuwataka wale ambao bado hawajakidhi vigezo wakamilishe taratibu husika.