Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhi zawadi ya Trekta kwa Chama cha Msingi cha Ushirika cha ISOWELU AMCOS kilichopo mkoani Njombe ikiwa ni kutambua juhudi za uzalishaji wa mazao kwa kiwango kikubwa zaidi kwa mwaka 2022.

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi trekta hilo kwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Chesko Ng'eve, wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kwanza ya Kimataifa ya Wakulima yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Akizungumza  mara baada ya kupokea Trekta hilo Mwenyekiti wa ISOWELU AMCOS Bw. Ng'eve amesema kuwa amefarijika sana kupokea zawadi hiyo kutoka kwa Rais kwani itakwenda kusaidia uchumi wa wana AMCOS kukua.

"Zawadi ina staha zake, nimejisikia vizuri sana kupokea zawadi kutoka kwa Serikali, zawadi ambayo itakwenda kukuza uchumi wa Chama, nimejisikia furaha sana sana tena mno, kitendo cha kutangazwa kwamba ISOWELU AMCOS  wanapata Trekta  na mpokeaji ni Mwenyekiti Chesco Ng'eve, ilikuwa ni furaha mno sio kidogo," amesema Mwenyekiti.

Aidha, Mwenyekiti ameishukuru Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuwashauri na kuwapa mafunzo, hasa ya MUVU ambayo yamewasaidia sana kufikia hatua hiyo.

"Naipongeza sana Tume ya Maendeleo ya Ushirika, lakini sisahau wakulima kule kuelewa yale sisi tunayaona kama viongozi kuyapokea na kuyafanyia kazi," amesema Chesco.