Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesema ataulinda na kuutetea Mfumo wa Ushirika popote kwa kuwa ndiyo mkombozi kwa watu wanyonge.

Mhe. Bashe amesema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) kwa mwaka 2022 yaliyofanyika mjini Tabora kwa siku tano kuanzia tarehe 28 Juni, 2022 hadi leo tarehe 02 Julai, 2022.

"Nitaulinda na kuutetea Ushirika popote pale kwa kuwa ndiyo mkombozi wa Mtu mnyonge, awe mkulima au Mjasliamali yeyote; Ushirika kama Mfumo hauna matatizo, tatizo ni baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika," amesema Mhe. Waziri.

Mhe. Waziri Bashe amewataka Wanaushirika kuchagua Viongozi miongoni mwa Wanaushirika wenyewe, wakiwemo wakulima wanaouza mazao yao kwenye Vyama vya Ushirika. Wanaochaguliwa lazima wawe wabunifu na waaminifu.

"Kama Mimi ni mkulima nipewe haki ya kuchaguliwa, kuchagua Viongozi ninaowataka na kupata taarifa kwenye Chama changu cha Ushirika," amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amesema Serikali imedhamiria kufufua  ginery za kuchambua Pamba zinazomilikiwa na Vyama vya Ushirika ili kuongeza thamani ya zao la Pamba na mazao yake.

"Lazima tuanze Safari ya Kuongeza thamani ya mazao yetu, tuchague Viongozi ambao ni Wanaushirika wenzetu na wenye uchungu na Mali za Ushirika," ameeleza Mhe. Bashe.

Vilevile, Mhe. Bashe amesema Serikali imedhamiria  kutengeneza taasisi ya fedha ambayo itatunza fedha za Wanaushirika wakiwemo wakulima na wajasliamali wengine; Taasisi hiyo ni Benki ya Taifa ya Ushirika.

 "Benki ya Ushirika itatumika kama jukwaa la Majadaliano kati ya Wanaushirika na taasisi za fedha na kuwawezesha wanaushirika kupata faida kwenye akiba wanazoziweka kwenye Benki hiyo," amesema Waziri.