Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka Wasimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Vyama ili kusimamia mali na fedha za Wanaushirika kwa lengo la kuwawezesha Wanachama kunufaika na Huduma zinazotolewa katika Vyama hivyo.

Naibu Waziri ametoa wito huo wakati akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yaliyoanza tarehe 28 Juni, 2022 Mjini Tabora ambapo Wanaushirika nchini kote wamekutana kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Ushirika nchini.

Naibu Waziri Mavunde ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kuimarisha Mfumo wa Kanzidata na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika na Wanaushirika nchini, kusimamia na kuratibu kwa ukaribu  uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika.

Aidha. Mhe. Mavunde amelielekeza Shirika la Ukaguzi na Usimamizi  wa Vyama vya Ushirika (COASCO), kuendelea kuimarisha Mifumo ya Udhibiti  na Usimamizi wa mali zikiwemo fedha ya Vyama vya Ushirika.

Mhe. Mavunde amekitaka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), kuendelea kutoa elimu ya Ushirika  kwakuwa wananchi wengi na Wadau  hawajajua Ushirika na  umuhimu wa kujiunga na Vyama vya Ushirika.

Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limetakiwa kuhakikisha kuwa linatoa huduma kwa Vyama vya Ushirika ikiwemo mafunzo, masoko, utafiti na ushauri wa namna bora ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika.