Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amevitaka vyama vya Ushirika kuongeza uzalishaji ili kufanya vyama viongeze tija kwa kuongeza wigo wa kibiashara na manufaa  Kiuchumi.

Mrajis ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya kikazi kwenye miradi mbalimbali ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Juni 27, 2024.

Amesema Vyama vya Ushirika vitumie rasilimali zilizopo vizuri kwa malengo ya kuongeza vifaa vya kitaalamu vitakavyoongeza uzalishaji ikiwemo matrekta na zana nyingine za kilimo, pamoja na kulima mazao kwa misimu zaidi ya moja hasa katika Skimu za Umwagiliaji ili kuongeza faida kwa Wanaushirika.

Aidha, ameshauri Wanaushirika kupanua wigo wa masoko kwa kujitangaza, kukuza mahusiano na Vyama vingine ndani na nje ya nchi, kuwa na Tovuti, kutumia Mitandao ya kijamii pamoja na kuangalia fursa za mazao yaliyopo katika mnyororo wa thamani wa mazao wanayolima ili kuongeza mapato.

“Mfano kwenye zao la Mpunga Wanaushirika wasiangalie mchele peke yake kuna fursa zingine ya zao inayoweza kutumika kama vile Pumba kuuzwa kwaajili ya vyakula vya wanyama pamoja na mbolea,” amesema Dkt. Ndiege .

Pia amevitaka Vyama Vikuu vya Ushirika kuongeza kasi ya kuanza kutumia Mizani za kidijitali kwa vile ambavyo bado havijaanza matumizi ya mizani hizo.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu Igembensabo, Joseph Ngeliya, amesema Mikakati ya Chama hicho ni pamoja na kuanzisha Kiwanda cha kuchakata Pamba na tayari hatua za awali zimeshaanza.

Mrajis amefanya ziara katika Mashamba ya Mpunga ya Skimu za Umwagiliaji za Mwamapuli zenye Hekta 630, maghala ya Chama cha Ushirika Mwamapuli pamoja na Kituo cha ukusanyaji Pamba cha Igunga Balimi Amcos.

Pamoja na mambo mengine ziara hiyo ya Mrajis inafanyika ikiwa ni siku chache kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kuanzia Juni 29 na kilele kufanyika Julai 5, 2024 Ipuli Mkoani Tabora.