Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Zainab Telack amesema, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imemkomboa Mkulima wa Kilwa kwa kusimamia upatikanaji wa Mizani za Kidigitali  zinazowasaidia kupima Ufuta na hivyo kupunguza wizi uliokuwa ukifanyika katika Vyama vya Ushirika.

Amesema hayo leo tarehe 08/06/2023  wakati wa uzinduzi wa Mizani 85 za Kidigitali uliofanyika katika Chama cha Msingi cha Ushirika Tapwa kilichopo Wilaya ya Kilwa katika Chama Kikuu cha Lindi Mwambao.

Telack amepongeza Uongozi wa TCDC kwa mambo mazuri wanayofanya kwani mizani hiyo itamwezesha Mkulima kupata risiti inayoonesha jina la mkulima, idadi ya kilo zilizopimwa hivyo itasaidia sana Mkulima.

Aidha, Mheshimiwa Telack ametoa rai kwa wakulima kuacha kuuza kangomba na kupima Mazao yao kwa makopo kwani wanaibiwa bali wapeleke katika vyama vyao ili wauze kwenye mnada.

“Ufuta wa Lindi ni mzuri na unajulikana hata na wanunuzi hivyo ninaimani tutauza kwa bei nzuri zaidi ya maeneo mengine, wakulima acheni kuuza kienyeji mnajikosesha neema ambazo zinakuja,” amesema Mheshimiwa Telack.

Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushiriki Tanzania, Dkt Benson Ndiege amevitaka vyama vya Ushirika kuendelea kukusanya fedha ya kununua mizani kama ulivyokubaliwa kwa wakati ili mpaka kufika mwezi Seotemba mizani ziwe zimenunuliwa kwenye AMCOS zote na zianze kutumika katika msimu wa Korosho.

“Fedha zikipatikana zabuni itangazwe mapema kwani mizani hii ndiyo mwarobaini wa kuimarisha Ushirika  msimu wa korosho tunataka hizi mizani zitumike na wawe wamepewa elimu ya namna ya kuzitumia.

Ameeleza Dkt Ndiege mizani hii itasaidia kuwa na takwimu za wakulima na mazao wanayolima jambo ambalo litasaidia mkulima kuweza kupata huduma ya pembejeo kwa urahisi.