Watoa Huduma katika Vyama Vya Ushirika wametakiwa kuhakikisha mifumo yao inaunganishwa na Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika( MUVU).

Wito huo umetolewa na Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika - Udhibiti, Collins Nyakunga, leo tarehe 21/03/2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi baina ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Watoa Huduma wa TEHAMA katika Vyama Ushirika wa Akiba na Mikopo.

 Naibu Mrajis ameeleza kuwa uwepo wa muunganiko wa Mifumo yao na mfumo wa MUVU utasaidia  kujua namna watoa huduma hao wanavyofanya kazi katika Vyama vya Ushirika kwa kila siku na itaonesha uwazi na ufanisi wa watoa huduma hao.

Aidha, Naibu Mrajis ametoa onyo kwa watoa huduma ambao wanasajiliwa kutoa huduma katika Vyama vya Ushirika na wanaharibu kwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu alafu wanaenda kufungua kampuni nyingine na kuomba usajili upya baada ya kuwa wamefungiwa kampuni iliyoharibu mwanzo.

“Huu mnaofanya ni udanganyifu mpaka umefungiwa kutoa huduma kwenye Vyama inamaana wewe si muaminifu na si mtu wa kufuata utaratibu hivyo acheni kufungua kampuni nyingine tukikubaini tutakuchukulia hatua kali,” amesema Nyakunga.

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi anayesimamia vyama vya kifedha, Josephat  kisamalala, amesema Tume haina mpango wakuendelea kufanya kazi na watu ambao hawatumi mifumo kwasababu kuendelea kufanya kazi bila kuendana na kasi ya kiteknolojia ni kujichelewesha kimaendeleo na mifumo yao lazima iunganushwe na ya Ushirika.