Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 08 Agosti, 2023 ametembelea Kijiji cha Ushirika na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania,Wadau na Wanaushirika kwa ujumla.

Akiwa katika Kijiji cha Ushirika Dkt. Samia alielezwa na Mrajis wa Vyama Vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson Ndiege kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na wadau wa Kijiji cha Ushirika waliokuwepo katika Maonesho ya Kwanza ya Wakulima ndani ya Kijiji cha Ushirika katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuiongezea nguvu Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) ili kuweza kuwasaidia Wanaushirika kuwa na benki yao (Benki ya Taifa ya Ushirika) kuwawezesha kupata mikopo kwa riba nafuu.

"Na leo wakati nazunguka mabandani niliingia katika kijiji cha Ushirika, wameniambia mikopo kupitia mabenki inawapa usumbufu kidogo kwa maana hiyo wanaanzisha benki yao, sasa TADB jikung'uteni kidogo muunge juhudi za washirika ili Ile Benki yao iweze kusimama vizuri," amesema Mhe. Rais