Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kutumia mifumo ya Kidijitali katika uendeshaji na uchakataji wa taarifa za Wanachama ili kuboresha utendaji na utunzaji wa Taarifa za Kifedha.
Mrajis ametoa kauli hiyo leo Juni 21, 2024 Jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa TEHAMA wa Muungano wa Vyama vya Ushirika wa kifedha SCCULT (1992) Ltd kwaajili ya uendeshaji na utoaji huduma za Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).
Akiongea katika uzinduzi huo ameelekeza Muungano wa Vyama vya Ushirika wa kifedha (SCCULT), Mfumo huo kuwa na uwezo wa kusomana na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) Mfumo unaosimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tume inapata taarifa za Vyama kwaajili ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Ushirika.
Akisisitiza kuwa utekelezaji wa uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ni sehemu ya maono makubwa ya Serikali ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inahitaji Vyama vya Ushirika kuwanufaisha Wanachama na kukuza Uchumi. Hivyo, TEHAMA kutumika kama chachu ya kuongeza tija, uwazi na kasi ya uchumi.
Makamu Mwenyekiti wa SCCULT, Kolimba Tawa, amesema Mfumo huo unaenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa Taarifa za Vyama, itaongeza uwazi na uwajibikaji kutokana na taarifa kuchakatwa na zaidi ya mhusika mmoja, kutengeneza ripoti zinazohitajika na wadau kwa wakati pamoja na upatikanaji wa kumbukumbu hasa panapojitokeza changamoto.
Mfumo huo wa TEHAMA wa Muungano wa Vyama vya Ushirika wa kifedha SCCULT (1992) Ltd umeundwa kwa kushirikisha Kampuni ya UBX, Umoja Switch, DSIK pamoja na Vyama mbalimbali vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).