Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw.Frank Kanyusi, amesema kuwa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa kielekroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) utarahisisha utoaji huduma katika Vyama vya Ushirika kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kuhusu matumizi ya Mfumo huo yaliyoanza leo tarehe 11/01/2023; Bwana Kanyusi amesema kuwa TEHAMA ni njia rahisi inayowawezesha watendaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Wanaushirika kwa ujumla kupata taarifa mbalimbali katika utendaji wa kazi pamoja na kupata taarifa za wakulima walioko kwenye vyama vya Ushirika.

Washiriki wa mafunzo haya ni Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa, Maafisa Ushirika, Mameneja na Wenyeviti wa vyama Vikuu vya Ushirika kutoka mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

"Mfumo huu utakwenda kutoa fursa kwa Tume,Vyama vya Ushirika pamoja na wadau wake kuwasiliana pamoja na kutekeleza majukumu yake kupitia mfumo huu; hivyo niwaombe washiriki wa mafunzo haya kuzingatia yale yanayoelekezwa ili kuweza kwenda kutekeleza kazi kwa ufanisi zaidi.

Naye Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania,  Bw.Valency Karunde amesema kuwa mfumo huu utapunguza ubadhilifu katika Vyama vya Ushirika.

"Bila taarifa ina maana hata udhibiti  wa shughuli za Vyama vya Ushirika unakuwa ni mgumu, hivyo kupitia Mfumo huu ni rahisi kupata upatikanaji wa taarifa kupitia kwenye vyama vya Ushirika," alisema Karunde.

Vilevile Bw.Karunde amesema kuwa Mfumo huu utapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za Ushirika; ambapo wakulima wa vijijini hawatahitajika kusafiri kwenda katika ofisi za Wilaya au Mkoa kupata taarifa juu ya ununuzi na uuzaji wa mazao, badala yake watazipata kupitia mfumo huu.

Mwenyekiti wa TANECU LTD Bw. Karimu Kipole, ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ameishukuru Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa  kutoa mafunzo kuhusu Mfumo ambayo yatawasaidia kufanya kazi kwa urahisi na kwa ufasaha zaidi na kuweka uwazi katika utendaji kazi.

"Kupitia mafunzo haya tunaamini kuwa kila kitu tutakachokwenda kukifanya kitakuwa bayana, pia mfumo huu utasaidia sana kuondoa watendaji wabadhilifu," amesema kipole.

Ameongeza kuwa viongozi wa Vyama vya Ushirika watahakikisha mafunzo haya yanawafikia Watendaji wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote.

Mafunzo haya ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika tayari yamefanyika kwa mikoa ishirini na sita ya Tanzania Bara ambapo washiriki wa mafunzo haya ni Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa, Maafisa Ushirika, Mameneja na Wenyeviti wa vyama Vikuu vya Ushirika.