MCHAKATO WA UANZISHWAJI BENKI YA USHIRIKA  UFANYIKE MAPEMA - DKT. ISHENGOMA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Ufugaji na Maji,  Mhe. Dkt. Christine Ishengoma amesema; ili kuongeza tija kwenye  Ushirika ni vyema mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ukafanyika mapema iwezekanavyo kwa kuwa wazo la kuanzisha Benki ya Ushirika ni la Wanaushirika wenyewe, hivyo kufanya mchakato wake kuwa rahisi.

Dkt. Ishengoma ameyasema hayo alipokuwa akifunga Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani lililofanyika leo tarehe 1 Julai 2022 Mjini Tabora.

"Kwakuwa Serikali imeonyesha nia njema  ya kuhakikisha adhma hii ya uanzishaji wa Benki ya Kitaifa ya Ushirika  inakamilika; napenda kutoa wito wangu kwenu Wanaushirika, kununua Hisa katika Benki hii ya Ushirika," amesema.

“Katika kongamano la Siku ya Ushirika Duniani mmejadili mambo mbalimbali ikiwemo Mifumo ya Kodi, Stakabadhi Ghalani, matumizi ya TEHAMA na Mifumo ya Masoko, na Huduma za Fedha Pamoja na changamoto nyingi zinazowakabili Wanaushirika; lengo kuu la mijadala hii ni kuona jinsi ambavyo Ushirika unaweza kusaidia kujenga ylimwengu Bora,” amesema Dkt. Ishengoma.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika  na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema kwa sasa Serikali imejikita kuendesha Vyama vya Ushirikai katika Mifumo ya kidijitali ili kuendana na kasi itakayoviwezesha vyama kupiga hatua kwa haraka.

Aidha, Dkt. Ndiege amewakumbusha Wanaushirika kuendelea kununua Hisa katika Benki ya Ushirika Kilimanjaro ili kufanikisha lengo la kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika.

Amevitaka Vyama vya Ushirika kuendelea kujenga Maghala katika Vyama vyao ili kuwawezesha na kurahisisha uuzwaji wa mazao yao, na kujenga viwanda vyao kufanikisha kuchakata mazao yao na kuwezesha mafaniko makubwa kwenye Sekta ya Kilimo.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Kuelekea Siku ya SENSA mwezi Agosti 2022, Kamishna wa SENSA na Spika Mstaafu, Mhe. Anna Makinda,  amewahimiza Wanaushirika  kushiriki kikamilifu katika zoezi Sensa ili kusaidia Serikali kujua Idadi ya watu wake ili kuwezesha kupanga Bajeti ya Taifa kwa usahihi.