Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, amezitaka Taasisi za Sekta za Huduma za Fedha kulegeza masharti ya mikopo ili kuweza kuwasaidia Wananchi kwa kupunguza riba za mikopo na hata wao  kupunguza gharama za matumizi yao ya kiofisi.

Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia katika Maonyesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Mkoani Mwanza alipokuwa akifungua Rasmi Maadhimisho hayo leo tarehe 24 Novemba, 2022 kwenye Viwanja vya Rockcity Mall.

Katika kuelegeza masharti hayo amewataka Watoa Huduma waangalie tena sharti la kuweka dhamana ya mali zisizohamishika kama nyumba kwani wapo watu wanakosa mikopo kwasababu hawana mali zisizohamishika.

“Wapo wanawake na vijana wanahitaji mikopo na ni wafanyabiashara ila wanashindwa kupata mikopo yenu kwasababu hawana nyumba mnapunguza idadi ya wateja kwasababu mtu akiwa na biashara ambayo inaonekana na ni halali biashara yake ni dhamana tosha,” amesema Makamu wa Rais Dkt Mpango.

Aidha, Makamu wa Rais  ameziagiza taasisi za fedha kuja na mkakati wa kuwasaidia vijana kwa mafunzo na hata mikopo ambayo  itawawezesha vijana hao katika kujiajiri ili kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira.

Dkt. Mpango amesema vijana wengi wamemaliza masomo wapo tu mtaani wanakosa sifa ya kukopeshwa kwasababu hawana ajira hivyo tafuteni namna ya kuwasaidia vijana hawa kuwapa mafunzo ya namna ya kujiajiri ili muisaidie Serikali katika kupunguza wasio na ajira.

Aidha, amezitaka Taasisi za Fedha kuendelea kutoa elimu ya fedha, elimu ya bima na elimu ya fedha kidigital (Emoney) ili kuweza kuwasaidia wananchi kuepeukana na utapeli wa mitandao.

“Huduma za kifedha ni Sekta mtambuka, lakini sekta hii inachangia chini ya asilimia 4 katika Pato la Taifa, ongezeni  ubunifu ili kuongeza mchango katika pato la Taifa,” amesema Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango amezitaka Taasisi za Fedha kupunguza gharama za kutuma fedha nje ya nchi ili kuepusha baadhi ya watu kutuma fedha kwa njia zisizo rasmi, hali inayosababisha kupotea kwa mapato katika Serikali yetu.