Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika anayesimamia Udhibiti, Colins Nyakunga amewataka Maafisa Ushirika kufanya kazi kama Maadili ya Kazi zao yanavyowaelekeza katika Utendaji.
Bw. Nyakunga meyasema hayo leo tarehe 16 Novemba, 2022 Jijini Dodoma katika ufunguzi wa kikao Kazi cha Wafilisi wa Vyama vya Ushirika vilivyofutwa katika Mikoa yote Tanzania Bara. Amesema kuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika kuanzia June 2020 hadi kufikia sasa, kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 100 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013, alifuta Vyama vya Ushirika 5,637 ambavyo vimeshindwa kufanya kazi kulingana na matakwa ya uanzishwaji wake.
Amewaelekeza Wafilisi walioudhuria kikao kazi hicho kuwa wakafanye kazi ya ufilisi kwa Vyama husika kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 na Sheria nyingine za nchi, na kuhakikisha kuwa wadai na wadaiwa wa vyama vilivyofutwa wanapata haki zao kwa wakati.
“Najua mtaweka mkakati mzuri wa kudhibiti kuwa na utitiri wa Vyama mwisho wa siku vinakuja kufutwa, kwahiyo najua kikao hiki kitaenda kuwa na manufaa kwa kuhakikisha kwamba mnakuwa Waadilifu pale mnaposhauri, Waaminifu pale mnapotoa maoni yenu na kutoa mapendekezo ya namna gani hivi vyama vinakwenda kusajiliwa, uendelevu wa hivi Vyama,” alisema Naibu Mrajis.