Mkuu wa Wilaya Kwimba ambaye anamwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Ng’wilabuzu  Ludigija amefungua Maadhimisho ya wiki ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mkopo Kitaifa Mkoani Mwanza leo tarehe 23 Oktoba, 2023 yenye kauli mbiu 'Wanachama Kusaidia Wanachama'

Mheshimiwa Ludigija ameeleza kuwa Ushirika umeundwa mahsusi kuhakikisha kila mwanachama anashiriki kumsaidia mwanachama mwingine kwa njia ya kukusanya kwa pamoja rasilimali na kuzitoa kama huduma ili  kulinda rasilimali hizi na kuhakikisha zinawanufaisha wengi.

Amevitaka Vyama vya Akiba na Mikopo kuimarisha huduma zinazotolewa na kuweka udhibiti wa ndani, masharti na Sera huku wakifuata Sheria na taratibu zote ili kuufanya Ushirika uendelee kuwa huru na kujisimamia.

“Hakikisheni mnajisimamia vema na maadhimisho haya yawe ni sehemu ya kujifunza na kupeana ujuzi, mkirudi katika maeneo yenu mzidi kuboresha Vyama vyenu pia endeleeni kufanya mambo yanayoigusa jamii moja kwa moja,” amesema Ludigija

Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amezitaka SACCOS kuendelea kuchangia kwa karibu kuimarika kwa mwamvuli wao (SCCULT) kwa kulipa Hisa, Michango ya mwaka pamoj na kuhakikisha wanawekeza kwenye mfumo wa kukopesha CFF uliopo SCCULT ili mfuko huo uweze kuwanufaisha na kuzikopesha SACCOS wanachama zenye changamoto ya ukwasi.