Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) kwa mwaka 2024 yatafanyika kuanzia tarehe 29/06/2024 hadi tarehe 06/07/2024 kwenye viwanja vya Nanenane (Ipuli) Mkoani Tabora ambapo wananchi wote vikiwemo Vyama vya Ushirika na wadau wote wa Maendeleo ya Ushirika wanakaribishwa kushiriki Maadhimisho hayo pamoja na kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Vyama vya Ushirika.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) kwa waandishi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 04 Juni, 2024 kuhusu maandalizi ya Maadhimisho hayo amesema kuwa lengo la Maadhimisho hayo ni kuwapa fursa wanaushirika kutangaza fursa zilizopo kwenye Ushirika pamoja na kupanua wigo wa ubia kati ya wanaushirika na wadau wake kitaifa na Kimataifa pamoja na kutafuta suluhu za changamoto za Ushirika.

"Kwa sasa tuna jumla ya Vyama vya Ushirika 7,446 vyenye jumla ya wanachama zaidi Milioni 8 vilivyosajiliwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi nchini. Vyama hivi vinasimamiwa kupitia Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ambapo shughuli zote za kila siku za Vyama hivyo vinaingizwa na kuonekana kwenye mfumo huo," amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis amesema kuwa kutakuwa na matukio mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani ikiwemo Kongamano la Elimu katika Vyama vya Ushirika, kongamano juu ya Hali ya  Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika, Kongamano la Fursa za Biashara na Uwekezaji kwa Vyama vya Ushirika na kongamano la Wanawake na Vijaya.

Aidha, Mrajis ameeleza kuwa  Sekta ya Ushirika inajivunia mafanikio makubwa ikiwemo uuzaji wa wazao ya wanachama kupitia mifumo shindani ambapo mzigo uliopo (mazao yaliyokusanywa) hutangazwa na wanunuzi wote kokote alipo hutoa bei na kushindanishwa. Hii imepekelea mazao ya wakulima kuongezeka kwa thamani ya mazao ya wakulima kwa bei iliyopo sokoni. Pia uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ambapo mpaka sasa Cheti cha usajili kimeshapatika na taratibu zingine zinaendelea ili benki hiyo iweze kuzinduliwa.