Wakulima wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani kwa pamoja wameridhia kuuza Ufuta wao kwa bei ya juu ya Shilingi 3,963/20 kupitia mnada ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo CORECU .

Mnada huo Umezinduliwa leo tarehe 7 Juni, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Micolas Kolombo katika ghala la Chama Kikuu CORECO. 

Mheshimiwa Kanali Kolombo amewataka wanunuzi waliouza ufuta huo kuhakikisha wanawalipa wakulima fedha zao kwa wakati ili waweze kufanya mambo ya maendeleo.

"Sitomvumilia kiongozi wa Vyama au mnunuzi anaechelewesha malipo ya Mkulima kwasababu kuchelewesha fedha hizo ni kumkwamisha Mkulima kuweza kufanya mambo aliyojipangia, tunataka kuona Kibiti inakuwa na majumba ya kifahali na biashara zinakuwa na fedha hizo hizo ndiyo zitaweza kufanya mambo haya mazuri," amesema Kanali Kalombo.

Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt Benson Ndiege amesema Mfumo wa Stakabadhi Ghala ndiyo mkombozi wa mkulima mmoja mmoja kutokana na Mkulima anachokipata kutokana na kuuza kwa mnada.

Dkt. Ndiege amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika kutunza takwimu zao vizuri ili Wakaguzi wanapofika waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa urahisi na pia Chama kikifanya hivyo kitajiepusha na Hati Mbaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Stakabadhi za Ghala Asangye Bangu, amewataka waendesha maghala  kuzingatia miongozo iliyopo na kujua mifumo hiyo ipo kwaajili  ya kusimamia jasho la mkulima.

Pia ametoa rai kwa Wakulima kusafisha ufuta wao na Viongozi wa vyama vya Ushirika kuhakikisha hawapokei ufuta ambao ni mchafu kwani unasababisha kuharibu soko la Mazao ya Tanzania.