Naibu Mrajis - Udhibiti,  Collins Nyakunga, amewataka Watendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) nchini kuhakikisha wanawasilisha taarifa za Vyama vyao ikiwemo kujaza madodoso yanayoitajika kwa ajili ya kuandaa taarifa ya Utendaji wa SACCOS na kuwasilisha taarifa hizo ofisi ya Mrajis mapema.

Nyakunga ameeleza hayo ili uandaaji wa taarifa hiyo ya mwaka 2024 iweze kuandaliwa na kuzinduliwa mapema. 

Ameeleza hayo Leo tarehe 13/02/2025 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma kwa lengo la kutathmini Taarifa ya utendaji wa SACCOS kwa Mwaka 2023 pamoja kufanya maandalizi ya uandaaji wa taarifa ya Utendaji wa SACCOS kwa Mwaka 2024.

Aidha, Naibu Mrajis ameeleza kuwa uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa SACCOS hautoishia tu kwenye SACCOS kwani sasa wasimamizi wa Vyama vya Ushirika ambavyo si vya kifedha wanaandaa taarifa ya Utendaji wa Vyama vya Ushirika ambavyo si vya kifedha.

Naye Mrajis Msaidizi - Usimamizi wa Vyama vya Ushirika wa Kifedha, CPA Josephat Kisamalala, ameeleza kuwa taarifa ya Utendaji wa SACCOS kwa Mwaka 2024 itakuwa ni taarifa ambayo imeboreshwa  zaidi kutokana na uwepo wa maandalizi ya uandaaji wa taarifa hiyo yameanza mapema kuliko ya miaka iliyopita.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa SCCULT(1992) LTD,  ADE Hassan Mnyone, ameeleza kuwa ili kufanikisha uandaaji wa taarifa hiyo ya Utendaji, ushirikiano unahitajika sana kwa wahusika wote wanaofanikisha uaandaji wa taarifa hiyo ili kuwezesha maandalizi ya taarifa husika. Hivyo, alisisitiza wadau wote washirikiane na kuwasilisha taarifa kwa wakati.

Kikao hicho kinafanyika kwa  siku mbili na kitajumuisha wataalamu kutokaTCDC, SCCULT (1992) Ltd, DSIK na Meneja wa SACCOS ambao wamewakilisha na Mameneja walioshiriki  Kikao kazi kutoka  BANDARIN, TANESCO, HAZINA na ELCT ND  SACCOS LTD SACCOS.