Ahadi ziwe kisheria na maandishi, kurahisisha ufuatiliaji Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika (UNION) kuhakikisha ahadi za bonansi zinazotolewa na   wanunuzi wa Mazao kuwekwa kisheria na kwa maandishi.

Amesema, ni jambo jema kwa kampuni hizo kusaidia jamii wanakonunua mazao kwa  kuwajengea ofisi, shule, au zahanati isipokuwa wanapotoa ahadi hizo ziwe ni  kwa maandishi ili iwe rahisi katika ufuatiliaji na kuhakikisha zimetekelezeka.

Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 03/02/2022 wakati wa kikao na  viongozi wa Mradi wa Pamoja wa Vyama vya Ushirika wa Tumbaku Tanzania (TCJE) na wenyeviti wa Vyama vya Ushirika vya KACU, WETCU, CHUTCU, MILAMBO na LATCU LTD kilichofanyika Jijini Dodoma.

Dkt Ndiege amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa kuhakikisha wanatoa elimu kwa Vyama ili wakulima waelewe madhara ya kuvunja mkataba uliosainiwa na ambao umebakisha kuingia kipindi cha mauzo pia wasiwe chanzo cha migogoro katika maeneo Yao. Vile vile, Dkt. Ndiege amesema vyama vya Ushirika vinapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia masilahi ya wakulima na wanachama wao bila kuvunja sheria wala upendeleo.

“Hembu jitahidi kabla ya kuanza kwa msimu mnapita kwa wakulima wenu mnazungumza nao mnachukua maoni na baada ya msimu kuisha rudini tena kwa wakulima mkazungumze nao mjue changamoto walizozipata na mzitatue ili mkiingia msimu unaofuata muwe mmemaliza changamoto za wakulima wenu,”  Dkt Ndiege alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa TCJE, Ntezilyo John, amesema watazingatia maagizo yaliyotolewa na Mrajis kwani kampuni zinazotoa ahadi ya bonansi zimekuwa haztimizi ahadi wanazotoa na hazipo kimaandishi. "Tunakaribisha kampuni nyingine kuja kununua Tumbaku Nchini na wanaotoa ahadi tunategemea watatimiza ahadi zao ili tuendele kufanya nao kazi kila msimu na tutaanza kufuatilia hizo ahadi," amesema Ntezilyo.