Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania,  Dkt. Benson Ndiege, amezindua  jengo la Ofisi ya Chama  Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao lililoghalimu shiling  416,904,460 ikiwa ni mapato ya ndani ya Chama hicho ikiwa ni gharama ya jengo na uzio wake.   

 Jengo hilo limezinduliwa tarehe 07 Desemba, 2023  ambapo Mrajis amesema Chama hicho kimeonesha mfano mzuri kwenye Vyama vya Ushirika kwa kuweza kujenga Ofisi ya kisasa kwa kutumia mapato yake ya ndani ambayo itaongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekeleza wa majukumu yao ya kila siku.

“Naimani kupitia mradi huu wa Ofisi yenu ya kisasa na sasa ikawe chachu kwa Vyama vingine vya Ushirika kuweza kujenga Ofisi zao. Pia nawaasa kutunza vizuri jengo hii ili liweze kudumu kwa muda mrefu na jengo  linahitaji mambo ya kidigitali tumieni sana mifumo katika kufanya kazi zenu,” amesema Dkt. Ndiege

Mrajis mesema  pamoja na maendeleo yanayofanywa na Chama Kikuu, vipo Vyama vya Msingi vimeweza kuanzisha miradi ya maendeleo kwa kujenga miundombinu mbalimbali kama ghala, ofisi na nyumba za kulala wageni na Vyama vingine vimeweza kununua malori na wanasafirisha mazao yao wenyewe kuyapeleka kwenye ghala na hivi ndiyo tunavyotaka Ushirika uwe.

Meneja Mkuu cha Chama cha Lindi Mwambao, Nurdin Swala, amesema ujenzi wa Ofisi yao ulifuata taratibu zote na kuridhiwa na bodi na wanachama. Ujenzi huo ulianza rasmi mwezi Machi 2022 na kukamilika Agosti 2023.

 Swala amesema jengo hilo litasaidia kuongeza tija kwa kuwahudumia wanachama na wadau wengine na kuongeza ufanisi wa kazi kwa watendaji na usimamizi wa bodi kwasababu mazingira ya jengo ni rafiki kwa kufanyia kazi.