Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo – Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi, ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuendelea kuimarisha na kuunda mifumo mbalimbali ya Kidigitali ili kudhibiti upotevu katika Vyama vya Ushirika na kuwahakikishia wanaushirika usalama wa fedha zao hasa wanapofanya mauzo ya mazao yao.

Ametoa agizo hilo  Desemba 19, 2024 alipoitembelea TCDC kwa leongo la kujitambulisha, kujifunza na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazoikabili pia kuskiliza maoni ya namna ya kutatua changamoto hizo.

Amemesema kumekuwa na njia mbalimbali za ubadhilifu wa fedha za wanaushirika hasa kwa kutoa takwimu zisizo sahihi na ujanja mwingi ambao unapelekea ushirika kuonekana sio sehemu sahihi ya uwekezaji na kukwamisha maendeleo ya Ushirika, hivyo mifumo itasadia kukomesha ubadhilifu na kuongeza mapato ya serikali.

“Kuna baadhi ya mikoa wamekuwa wakitoa takwimu zisizo sahihi za wanachama, hasa wakati wa ugawaji wa pembejeo za kilimo na ujanja mwingi na ukwepeshaji wa fedha za serikali, hivyo natoa agizo iundwe mifumo ya kuwahakikishia wanachama wa vyama vya ushirika usalama wa fedha zao,” amesema Dkt. Nindi.

Aidha, aliisisitiza Tume kuandaa na kushiriki kwenye makongamano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali kuhusu ushirika ili kuboresha uendeshaji wa vyama hivyo kwa maslahi mapama ya Taifa.

Vilevile Dkt. Nindi, ameipongeza TCDC kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuhakikisha Ushirika unaaminika tena na wananchi ikiwemo kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Vyama Vya Ushirika (MUVU) na upimaji wa mazao ka kutumia Mizani ya Kidijitali na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanafikia malengo ya Serikali.

Naye, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndeige, ameishukuru Serikali katika kuboresha na kuimarisha Ushiirika Nchini na amesema TCDC itaendelea kutekeleza maagizo yaliotolewa serikali kwa lengo la kuimarisha Ushirika.