Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo - Ushirika & Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi amevitaka Vyama vya Ushirika kuongeza ubunifu wa uendeshaji wa shughuli za Ushirika ili kuinua tija na uzalishaji mali wenye matokeo chanya kwa Wanaushirika na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Nindi amesema hayo wakati wa kikao na Wajumbe wa Bodi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Kilimanjaro KNCU (1984) LTD akiwa katika ziara ya kikazi Mmmkoani Kilimanjaro iliyoanza leo Machi 6, 2025.
Akiongea na Wajumbe hao amesema ni muhimu kwa Viongozi wa Ushirika kuwa wabunifu katika kutumia rasilimali za Vyama vya Ushirika kibiashara ili vyama viweze kujiendesha kiushindani na kuzalisha faida kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo ikiwemo kuongeza matumizi ya Mifumo ya TEHAMA, kushirikisha Wadau wa kuendeleza Miradi ya Vyama pamoja na usimamizi mzuri wa mali za Ushirika.
“Fursa za Ushirika ni nyingi kupitia miundombinu iliyopo hivyo tuzitangaze fursa hizo ili wawekezaji na Wadau waweze kushirikiana na Vyama vya Ushirika kuongeza tija kwa kujiendesha kibiashara,” amesisitiza.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ametembelea Miradi mbalimbali ya KNCU ikiwemo Mgahawa wa Kahawa, eneo la Maghala ya Chama, Kiwanda cha kukoboa Kahawa (TCCCo Ltd), Shamba la zao la Vanilla linaloendeshwa na Kampuni ya Vanilla Natural Extract inayoshirikiana na Vyama vya Ushirika.
Katika ziara hiyo leo Naibu Katibu Mkuu amekutana na Viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo, Kiseo Nzowa kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kuongeza tija ya Ushirika Mkoani hapo.