Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro amepongeza Menejimenti ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kwa ufanyaji kazi wao wa kufuata kanuni na miongozo ya kiutumishi.

Ametoa pongezi hizo leo tarehe 30/11/2022 wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Maendeleo ya Ushirika uliofanyika Jijini Dodoma.

Dkt. Ndumbaro amesema Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume pamoja na Menejimenti yake imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi walio katika Ushirika kupata haki na stahiki zao kwa wakati.

“Mnafanya mambo mazuri malalamiko yamepungua kwa wakulima wanaouza mazao yao kwa Stakabadhi za Ghala maana wanapokea fedha za malipo yao kwa wakati, huu ndiyo utumishi unaohitajika katika Serikali yetu,” amesema Dkt Ndumbaro.

Vile vile, Dkt Ndumbaro amewakumbusha watumishi wa Tume kuzingatia Uadilifu, Uwajibikaji, Bidii na Ubunifu pamoja na Haki kwani hizi ndiyo nguzo kubwa katika Utumishi wa Umma na zikizingatiwa kila mwananchi atapata huduma iliyo bora na yenye uhakika.

Aidha, Dkt Ndumbaro ameitaka TCDC kuhakikisha wakulima wanaacha kuuza mazao yao yakiwa shambani kwa kuwa na mpango wa kuanzisha SACCOS ndani ya AMCOS ambao utamlinda mkulima na kumsaidia kupata fedha pale wanapokuwa na uhitaji.

“ Hivi mnafikiri wakulima wetu wanapenda kuuza mazao yao kwa bei rahisi kabla ya kuyatoa shambani? Hapana ni shida ndiyo zinawafikisha hapo walipo sasa wasaidieni waache tabia za kuuza maua au mazao kabla ya kuvuna," amesema Dkt Ndumbaro.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege amemuomba Katibu Mkuu kuipa kipaumbele na kuitazama Tume kwa jicho la kipee kama Taasisi ya kimkatati ili iweze kufanikisha mikakati na ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kuhudumia Sekta ya Ushirika.

Dkt Ndiege amesema Vyama vya Ushirika vimechangia kiasi kikubwa katika ongezeko la pato la Taifa na kwa mwaka 2019/2020 hadi 2021/ 2022 jumla ya tani 9, 804, 347 za mazao ya kimkakati ziliuzwa kupitia Vyama vya Ushirika na jumla ya shilingi    2,917,816,152,983.61 zililipwa kwa wakulima na Serikali imepata tozo za kodi mbalimbali kupitia mamlaka zake.
 
“Mamlaka za Serikali za Mitaa katika mwaka 2021/2022 zimepokea jumla ya Tshs 15,144,077,319 zikiwa ni fedha za ushuru unaotokana na zao la Korosho uliolipwa na Vyama vya TANECU, MAMCU,  RUNALI, LINDI MWAMBAO, TAMCU NA CORECO na pia jumla ya  Tshs 1,041,957,051.00 zimepokelewa Kama ushuru kutoka Vyama vya KDCU NA KCU kupitia zao la Kahawa," amesema Mrajis.

Ushirika inafanya mambo makubwa ambayo yanachagia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la la Pato la Taifa na ndiyo maaan kuna Viwanda Vidogo, Kati naa Vikubwa 279 vimeanzishwa chini ya Mfumo wa Uendeshaji wa Vyama vya Ushirika. Amesema Ndiege.

Awali, Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania walichagua Katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza hilo. Waliochaguliwa ni Selestina Kinoge kuwa Katibu na Albert Mwombeki kuwa Katibu Msaidizi.