Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ametoa rai kwa Maafisa Ushirika Nchini kuwa waadilifu na kuziba mianya ya rushwa katika Utendaji kazi wao.
Amesema uadilifu na maadili kazini ni jambo ambalo kila mtumishi anapaswa kulizingatia, ili kila mtumishi aweze kutekeleza wajibu wake na kuimarika katika utendaji kazi baada ya kupata mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika kwa maafisa.
Amesema hayo tarehe 01/03/2025 wakati wa kufunga mafunzo ya Usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa Maafisa Ushirika wa Kanda ya Kaskazini mjini Babati - Manyara ambapo Maafisa 116 wamepata mafunzo hayo.
Dkt Ndiege amesema Ushirika ni sekta ambayo inagusa wananchi moja kwa moja, hivyo Maafisa Ushirika wanapaswa kuzingatia uadilifu na kukuhakikisha wanaziba mianya ya rushwa katika utendaji kazi wao.
“Niwaambie tu rushwa ni adui wa Ushirika, zuieni mianya ya rushwa na jiepusheni na rushwa msijitie doa kwa mambo yanayoepukika,” amesema Dkt. Ndiege
Aidha, Dkt Ndiege amesema anategemea Maafisa waliopata mafunzo wataenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata na wataishi ndani ya hayo mafunzo ili kuboresha Utendaji kazi wao wa kila siku.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Maafisa Ushirika, Sofia Shoko, ametoa shukurani kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuweza kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajenga na kuwaongezea ufanisi na weledi katika utendaji kazi wa kila siku.
Shoko amesema kuwa kupitia mafunzo waliyopata washiriki wakirudi katika maeneo yao ya kazi kutakuwa na mabadiliko makubwa katika kutekeleza majukumu yao.