CRDB na NHIF Zaingia Mkataba wa Makubaliano Kuboresha “Ushirika Afya”

Dar Es Salaam,

Benki ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kurahisisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wakulima ambapo ushirikiano huo utawawezesha wakulima kupata bima ya afya za NHIF kwa mkopo. Huduma hiyo ambayo imepewa jina la “Ushirika Afya Premium Loan” itatolewa kwa wakulima ambao wapo katika vyama vya ushirika huku pia ikiwanufaisha wategemezi wao, kwa maaana ya mke/ mume na watoto.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa huo wa makubaliano imefanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Mei, 2021 kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga; na kushuhudiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema katika makubaliano hayo Benki ya CRDB itakuwa ikisaidia kulipa gharama za bima ya afya (premium) na wakulima kulipa mwisho wa msimu baada ya kuuza mazao yao.

“Mkopo hutolewa kulingana na kiwango cha gharama za malipo ya bima ya afya (premium) ambapo kwa mtu mzima ni shilingi 76,800 na mtoto shilingi 50,400,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa mkopo huo wa bima ya afya utatolewa bure bila ya makato wala riba yoyote.

Kupitia huduma hiyo ya “Ushirika Afya Premium Loan”, Mkulima pia anaweza kuchukua kifurushi cha familia cha malipo ya shilingi 355,200 ambapo atapata bima ya afya kwa watu 6 (watu wazima 2, watoto 4). Kifurushi hiki kimeanzishwa ili kuhamasisha wakulima kukata bima kwa familia zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, amesema kuwa, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umejipanga kuhakikisha unawahudumia kikamilifu wakulima ili wawe na uhakika na shughuli zao za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.

“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwawezesha wakulima wawe na uhakika wa afya zao kwa maana ya kupata huduma za matibabu wakati wowote wanapozihitaji na kwa upande wa Mfuko tumeboresha zaidi huduma zetu ili mwanachama wetu asipate usumbufu wa aina yoyote,” amesema Konga.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango huu, Mrajis wa Vyama vya ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amezipongeza CRDB na NHIF kwa kuwajali wakulima na kuwapatia uhakika wa matibabu wakati wote kupitia “Ushirika Afya Premium Loan”.

“TCDC ipo tayari kushirikiana na Wadau wenye nia njema ya kuendeleza Wanaushirika katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo afya na nyinginezo. Tutashirikiana na yeyote mwenye dhamira ya kweli kumnufaisha Mwanaushirika na hatutasita kuchukua hatua kwa yeyoye atakayekwenda kinyume na Sheria na taratibu zilizowekwa,” amesema Dkt. Ndiege.

MWISHO