Wanachama wa Chama cha Ushirika wametajwa kuwa ndio wamiliki wa kwanza wa Chama cha Ushirika. Hivyo, wana wajibu wa kulinda na kusimamia Chama cha Ushirika kuendeshwa kwa tija kwa maslahi ya Wanachama wote wa Chama cha Ushirika.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Mussa Musaile akifunga mafunzo yaliyoratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi wa Vyama vipya vya Ushirika kutoka Halmashauri za Wilaya za Karatu, Meru na Arusha wanaolima mazao ya Mbogamboga, matunda na mazao mchanganyiko yaliyoanza Juni 5, 2023 na kuhitimishwa Juni 6, 2023 Mkoani Arusha.
Katibu Tawala amewaasa Viongozi kwenda kusimamia na kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha kwamba wanasimamia wanachama wao kutimiza wajibu wao ikiwemo ulipaji wa hisa utakao changia katika kujenga na kuimarisha mtaji wa Chama, kulipa viingilio, kushiriki wa Mikutano mikuu, Chaguzi za Vyama pamoja na majukumu mengine yaliyowekwa kwa mujibu wa Sheria na Masharti ya Chama.
“Vyama vya Ushirika vinamilikiwa na wanachama wenyewe, hivyo ili kuhakikisha vyama hivi vinakuwa imara na endelevu ni lazima kila mwanachama ahakikishe anamaliza hisa kwa mujibu wa Sheria na Masharti ya Chama ili kuweza kujenga mtaji wa ndani wa chama na kuwa imara kiuchumi,” alisema
Aidha, Katibu Tawala amewasihi Viongozi hao kutumia maarifa waliyopata kutekeleza kwa vitendo na kuhakikisha wanachama wanaendeleza kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao mchanganyiko kwa maendeleo yao wenyewe na kwa jamii inayowazunguka. Akaongeza kuwa kupitia Vyama vya Ushirika Wajumbe wa Bodi watumie fursa za zilizopo katika Kilimoikiwemo masoko, makongamano, ziara za kibiasharana pembejeo za kilimo kwa ustawi wa Vyama vya Ushirika.
Awali akiongea kwa niaba ya washiriki wa mafunzo John Mangi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya masuala ya Kilimo pamoja na kuusimamia Ushirika Mshiriki huyo amesema Wanaushirika wana matarajio makubwa ya upatikanaji wa masoko kupitia Ushirika hususani kwa mazao yanayozalishwa na wakulima wa mazao ya Mbogamboga, matunda na mazao mchanganyiko. Hivyo, wajumbe hao wataenda kuzingatia masuala mbalimbali yaliyofundishwa kwa lengo la kuwa na Ushirika imara.
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa wanaushirika ili kuimarisha na kusimamia Ushirika pamoja na uwezekano wa kuongeza mbolea ya Ruzuku kwa Wakulima hususani kwa maeneo yaliyo mbali na miji sambamba na mbolea hiyo kuzingatia aina ya zao na eneo la kilimo.
Aidha, mshiriki huyo ameiomba Serikali kujenga miundombinu ya maghala ya kisasa, mashine za kuchakata na kusindika mazao, miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji na Barabara kwenye maeneo ya mashamba.
Jumla ya Vyama vya Ushirika wa mazao ya Mbogamboga, matunda na mazao mchanganyiko 14 vimeanzishwa mkoani Arusha ambapo Wajumbe wa Bodi wapatao 86 wamepata mafunzo. Timu za wataalamu kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo, Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), TAHA, wametoa mada mbalimbali ikiwemo dhana ya Ushirika, Sheria ya Vyama vya Ushirika, Wajibu wa Wajumbe wa Bodi, Maadili ya Uongozi, Uendeshaji wa Mikutano Mikuu ya Vyama, Uandaaji wa makisio ya mapato na matumizi ya Chama pamoja na upatikanaji wa pembejeo.