Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pamba, Marco Mtunga, ameshauri Bodi za Mazao na Taasisi za utafiti wa Kilimo kuhakikisha wakulima wanakuwa na mfumo wa kidigitali ambao utamsaidia mkulima katika kuuza mazao yake na kupata pembejeo kwa wakati na kuwahamasisha wakulima hao kujiunga na kujisajili katika Mfumo huo.

 Bwana Mtunga amesema mfumo huu unapaswa uwe na kadi za kidigitali ambazo zitamtambulisha mkulima, shamba lake na mazao anayolima na pia kadi hiyo  ndiyo impe uhalali wa kuuza mazao yake.

Amesema hayo leo wakati wa kikao kilichohusisha Taasisi za Utafiti wa Kilimo na Bodi za Mazao kuhusu namna ya kudhibiti ongezeko la Magonjwa na Wadudu waharibifu wa Mazao kilichofanyika katika ukumbi wa Posta Morogoro Mjini.

Bwana Mtunga amesema kutakapokuwa na mfumo huo na kadi hizo itakuwa rahisi mkulima kupewa viwatilifu na mbolea kwa wakati na kulipa kwa wakati kwasababu mfumo wa kidigitali utakuwa unasimamia kila kitu.

Aliendelea kusema kuwa kadi hizo zitatakiwa ziwe uwezo wa mkulima kukatwa pesa ya viwatilifu na mbolea za ruzuku alizopewa na mfumo uwe na namna ya kumlipa mtoa pembejeo wakati huo huo.

“ Naipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanzisha mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ambao unampa mwanya Mrajis wa Vyama vya Ushirika kuweza kuona namna vyama hivyo vinavyofanya kazi hivyo niwaombe bodi za mazao mkahamasishe vyama kuanza kutumia mfumo huu wa kidigitali ambao Mrajis atakuwa na uwezo wa kuona Vyama vyote vya Ushirika namna wanavyofanya kazi zao za kila siku na pia itapunguza mianya ya ubadhilifu” amesema Mtunga

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred, ameziomba Taasisi za Utafiti  wa Kilimo kutafuta namna ya kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima kwani uzalishaji umekuwa ni ghali katokana na ongezeko la  magojwa ya mazao ambayo yanapelekea matumizi ya viwatilifu kwa wingi.

“kila siku zinavyozidi kwenda magonjwa ya mazao yanazidi kuongezaka na kufanya wakulima kutumia gharama kubwa katika uzalishaji hivyo tunapaswa tushirikiane tuweze kuondoa hili tatizo kwasababu hali inavyoenda badala ya kusaidia kuongeza kipato kwa wananchi tutakuwa tunapunguza vipato vyao,” amesema Francis Alfred.