Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika Tanzania (CBT), Godfrey Ng'urah, amesema Benki ya Ushirika ipo sokoni sasa na itakuwa Benki itakayoongoza kutoa Huduma Bora za kibenki kidijitali na kuchochea  kasi ya ujumuishi wa huduma za kibenki na kifedha.

Mkurugenzi wa CBT ameyasema hayo Januari 29, 2025 kwenye mkutano na Wahariri na Wanahabari uliofanyika Jijini Dodoma. 

Mkutano huo wenye lengo la kuhabarisha Umma kuhusu Dira, Dhima na Adhma ya Benki ya Ushirika kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.

"Ndugu wanahabari, napenda kuujulisha Umma; Benki yetu ya Ushirika tayari imeanza kufanya kazi na itakuwa ni benki itakayoongoza kutoa huduma bora za kibenki kidijitali na kuwafikia watanzania wengi kwa mara moja, kwa urahisi, wepesi na  gharama nafuu," amesema Ng'urah.

Aidha, amesema katika kuhakikisha kuwa Dira, Dhima na Adhma za Benki ya Ushirika zinatekelezwa, itashirikiana kwa karibu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuhakikisha kuwa inachochea kwa kasi kubwa ujumuishi wa huduma za kibenki na kifedha na kuwafikia Wanaushirika wengi.

Ng'urah amesema kuwa Benki ya Ushirika kwasasa inamilikiwa na Wanaushirika kama wawekezaji Wakuu  pamoja na Vyama vya Ushirika (51%). Kwasasa Benki ya Ushirika imeanza kufanya kazi kwa matawi matatu ambayo ni Tandahimba, Moshi, na Dodoma.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Serikali  Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC ambaye alikuwa mgeni rasmi, Dkt. Benson Ndiege, ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika nchini kuendelea kufanya uwekezaji  kwenye Benki ya Ushirika ili wawe sehemu ya wanufaika wa Uwekezaji wa Benki hiyo.

Aidha, Dkt. Ndiege ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri wa Muunguno wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Benki ya Ushirika inaanzishwa kwa kutoa Mtaji wa Bilioni tano na kuwataka Watanzania katika Sekta zote za kiuchumi; Kilimo, Uvuvi, Biashara, Madini, Ufugaji, na makundi yote kufungua akaunti katika Benki ya Ushirika na  kunufaika na huduma bora ikiwemo mikopo ya riba nafuu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Ushirika, Prof. Gervas Machimu, amesema  Bodi inajivunia Mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la mtaji, huduma bora za kifedha na utoaji wa mikopo yenye riba nafuu. 

Vilevile amesema kuwa Bodi itahakikisha inasimamia kunakuwa na Mifumo salama ya kiutendaji na kusimamia Uadilifu na Uwajibikaji kwa kutumia Teknolojia za kisasa.