Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, amewataka Viongozi wa AMCOS kusajili mazao mengine yanayolimwa na wakulima katika Mikoa inayolima zao la Pamba.

Mheshimiwa Bashe amesema wanaosajili wakulima wa Pamba ni lazima wawasajili na wa mazao mengine yanayolimwa katika maeneo hayo ili iwape fursa wakulima kutambulika na kupata pembejeo.

Waziri BASHE ametoa kauli hiyo leo tarehe 01/02/2023 wakati akipitishwa katika Mfumo Mpya wa Mauzo ya Pamba wa Kidigitali, Jijini Dodoma.

Mhe. Bashe amesema kipindi hiki ambacho wanasubiri muda wa mavuno na minada, Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na TCDC na Bodi ya Stakabadhi za Ghala kuanza kupeleka vifaa na kuwapa elimu wakulima na viongozi wa AMCOS namna ya kutumia Mfumo huo.

“Anzeni kutoa mafunzo ili lisije kuwa ni jambo la kushitukiza kwa wakulima ili wawe na uelewe nini kinaenda kufanyika na Mimi na Naibu wangu tutafanya ziara katika maeneo hayo kufuatilia mwenendo wa haya ninayoyaagiza,” amesema Mhe. Bashe.

Aidha, Mhe. Waziri ameelekeza  'bidding' kwa wafanyabiashara zitafanywa 'online' kila siku baada ya makusanyo ya Pamba kwa masaa nane na saa Tisa mchana bei ya juu itakayopatikana kwenye kila kituo cha mauzo ndiyo wakulima wanakuwa wameuza na kupatiwa fedha zao.

“Mkulima akipima mzigo wake apewe risiti ya kukabidhi mzigo ghalani tu na baada ya mnada kukamilika basi mkulima awe ameuza Pamba yake kwa gharama iliyopatikana hivyo mnada uwe kuanzia saa 2 mpaka saa 9 mchana halafu ndiyo taratibu za mauzo ziendelee na mkulima apokee ujumbe wa mauzo yake kupitia simu yake,” amesema Mhe. Bashe

Akizungumza katika kikao hicho Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema Mfumo huu utamrahisishia mkulima kuuza  Pamba yake kwa urahisi na uharaka na mnunuzi atakuwa amepunguza gharama za kusafiri kwenda vituo vya ununuzi na ataweza kufanya 'bidding' popote alipo.

 Dkt. Ndiege amesema ili kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi, Bodi ya Stakabadhi za Ghala, Tume ya Ushirika na Bodi ya Pamba kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kuboresha  Mfumo wa mauzo ya mazao kwa lengo la kumsaidia mkulima aweze kunufaika na mazao anayozalisha.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wataalamu mliyofanya kazi hii na kuwashukuru kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kuandaa Mfumo huu ambao una lengo la kumsaidia mkulima; tuendelee kushirikiana ili wakulima waweze kupata huduma iliyo bora zaidi,” amesema Dkt. Ndiege