Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema Benki ya Ushirika Tanzania itakuwa ni Benki ambayo itaongozwa na misingi ya Kibiashara ili kuleta tija na maendeleo kwa Wanaushirika na Taifa kawa ujumla.

Waziri Bashe amesema hayo akifungua Mkutano Mkuu wa kwanza wa Benki ya Ushirika (CBT) Oktoba, 17, 2024 Jijini Dodoma, ambapo amewataka wasimamizi na watendaji wa Benki hiyo kuhakikisha Benki inafanya kazi kwa ufanisi utakaowezesha Benki hiyo kukua na kuingia katika Soko la Hisa ili kuongeza ukuaji na faida kupitia Ushirika.

Waziri Bashe ametoa wito kwa kuwa Vyama vya Ushirika, Taasisi za Kilimo na Wadau kufanya Biashara na Benki hiyo ili kukuza faida na Mapato ya Ushirika na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Benki hiyo kuiwezesha kukua na kuhudumia Wakulima na wadau wengine mbalimbali.

Aidha, Waziri amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunga mkono Wanaushirika na kuchangia Shillingi Billioni 5 katika mtaji wa Benki hiyo na kufikisha Shillingi Billioni 52.

Nae Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Abdulmajid Nsekela amesema Ushirika ni nyenzo inayoweza kutumika kugusa wananchi wengi hadi vijijini. Hivyo Benki hiyo inakwenda kuongeza kasi ya kufikisha huduma za kifedha kupitia mikopo na huduma nyingine za Kibenki.

Ameongeza kuwa Tume inaunga mkono dhana ya kuendesha Benki kibiashara na kidijitali kwa kuvisimamia Vyama vya Ushirika kutumia Mifumo ya kidijitali inayoenda na kasi ya mabadiliko ya Kiteknolojia.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume Dkt. Benson Ndiege, Wenyeviti na Watendaji wa Vyama vya Ushirika, Viongozi wa Serikali na Wadau wa Maendeleo.