Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesisitiza umuhimu wa kuwapa vijana kipaumbele na fursa mbalimbali ndani ya sekta ya ushirika ili kujenga msingi imara wa kiuchumi na kuhakikisha uendelevu wa sekta hiyo kwa vizazi vijavyo.
Akizungumza leo, Agosti 7, 2026, alipotembelea Kijiji cha Ushirika katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma, Mhe. Nanauka ameeleza kuwa sekta ya ushirika ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu na vijana.
Mhe. Nanauka amebainisha kuwa ushirikishwaji wa vijana ni nguzo muhimu ya kuurithisha ushirika kutoka kizazi kimoja hadi kingine, akieleza kuwa kwa sasa sekta hiyo inatawaliwa zaidi na watu wenye rika kubwa ambao nguvu zao za uzalishaji zimeanza kupungua.
Kwa upande wake, Naibu Mrajis wa Uhamasishaji kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Consolata Kiluma, ameeleza kuwa Tume hiyo inaendelea na juhudi za makusudi za kuhamasisha vijana na wanawake kujiunga na Vyama vya Ushirika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Katika hatua nyingine, Kijiji hicho cha Ushirika kilipata fursa ya kutembelewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, aliyeambatana na viongozi waandamanaji wa wizara hiyo kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.




