Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) wamesema mafanikio makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika Sekta ya Ushirika yanaonyesha kuwa chachu ya kuongeza kipato cha wakulima, kupanua huduma za kifedha na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 5,2026 baada ya kutembelea mabanda ya Vyama vya Ushirika katika Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane, ambapo walieleza kuwa ushirika umeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Wakulima.
Kamishna Shaib Nnunduma, amesema Vyama vya Ushirika vinaendelea kuwawezesha wakulima kukusanya na kuuza mazao yao kwa pamoja, kupata masoko yenye tija na kuongeza thamani ya mazao. Alisema baadhi ya Vyama vimeanza kutoa huduma za usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji hadi masokoni, huku vyama vya kuweka na kukopa vikitoa fursa za akiba na mikopo inayowasaidia wanachama kuendeleza shughuli za uzalishaji na biashara.
Kwa upande wake, Kamishna Nkuvililwa Simkanga alisema ziara yao imebaini kuwa Vyama vingi vya Ushirika sasa vinaendeshwa kwa ufanisi na vinaanzisha miradi bunifu inayochochea maendeleo ya wakulima, wafugaji na wadau wengine wa uchumi. Aliwahimiza Watanzania ambao bado hawajajiunga na vyama vya ushirika kutumia fursa hiyo ili kunufaika na masoko, huduma za kifedha na fursa nyingine za kiuchumi zinazopatikana kupitia mfumo wa ushirika.
Naibu Mrajis ( Uhamasishaji) Consolata Kiluma aliongozana na Makamishna hao katika kutembelea Kijiji cha Ushirika




