Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesistiza umuhimu wa kutumia mifumo ya kidijitali katika kusimamia Vyama vya ushirika ikiwemo katika usambazaji wa mbolea kwa wakulima, usimamizi wa mali za Ushirika.
Dkt. Nchimbi ametoa rai hiyo leo Agosti 3, 2026 akiwa mgeni rasmi katika Siku ya Ushirika kwenye maonesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma.
Aidha, Dkt. Nchimbi amesema kuwa Kampeni ya "Linda Ushirika, Chagua Uadilifu" imekuja kwa wakati muafaka ili kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinafanya kazi kwa maslahi ya wanaushirika.
Pia, amehimiza Viongozi kuhamasisha Vijana na Wanawake kujiunga na Vyama vya ushirika ili kuendana na Dira ya 2050 kuinua Uchumi kwa watanzania wote.
Waziri wa kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Ushirika ni nguzo muhimu ya kuinua Uchumi wa mtanzania na kuwa nchi yetu bado inaaamini katika mfumo wa ujamaa na kujitegemea ambapo ndio nguzo muhimu ya Ushirika.
Akitoa taarifa ya hali ya Ushirika nchini, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC). Dkt.Benson Ndiege amebainisha kuwa mpaka sasa wanachama waliosajiliwa kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) wamefikia milioni 3.6.
Aidha, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vimeendelea kuwahudumia Wanachama wake Kwa kutoa Mikopo kufikia Shilingi trilioni 2.5.
Katika Siku hiyo maalumu kwa Wanaushirika, Makamu wa Rais alifanya Uzinduzi wa Taarifa ya mali za Ushirika na Mfumo wa huduma ya Bima kwa Wakulima kwaajili ya kuwasaidia wakulima kukata bima za mazao wanapopata na majanga kupata fidia.




