Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakulima kuhakikisha wanapeleka Kakao safi
katika maghala na waache kuchanganya na takataka kwani inaharibu sifa ya zao hilo inaposafirishwa nje ya nchi.
Ametoa wito huo leo Jumapili, Mei 12, 2024 wakati akizungumza na wananchi na wadau wa zao la kakao waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Chama Kikuu cha Ushirika cha Kyela (KYECU) mara baada ya kukagua ghala la kakao la chama hicho.
Waziri Mkuu amesema Kakao ya Tanzania ni bora hivyo Vyama visimamie uwekaji wa lebo katika magunia ya kila AMCOS ili wenye nia chafu ya kutaka kuharibu sifa nzuri ya zao hilo washindwe kwani itakuwa inajieleza imetoka wapi.
Vile vile amewataka Wakulima kuacha kuuza mazao yao majumbani au shambani bali wapeleke mazao hayo katika Vyama vya Ushirika ili waweze kuuza na kupata bei nzuri ambayo itamnufaisha zaidi mkulima.
“Kataeni wanunuzi wa majumbani hao ndiyo wanaoturudisha nyuma, Serikali inataka kila Mkulima anufaike na mnyororo wa faida ya kuuza kwenye Vyama anaekuja kukulaghai mwambie nenda kanunue kwenye Minada”
Amewataka wakulima wa zao hilo waendelee kuhakikisha mashamba yao yanakuwa masafi ili kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu. “Mashamba yenu hayana magugu ndiyo sababu mazao yenu hayana magonjwa. Endeleeni kusafisha mashamba ili kuzuia wadudu wanaoweza kuharibu zao hili,” amesema Mhe. Waziri Mkuu.
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde alisema wizara hiyo ina nia ya kuzalisha miche mingi ya mbegu ili iweze kugawiwa bure kwa wakulima. “Tumeomba tupatiwe eneo ili tuzalishe zaidi miche ya mbegu bora hadi kufikia 100,000 kutoka 34,000 ya sasa,” amesema Mhe. Silinde.
Wakati huo huo ulifanyika Mnada wa 47 wa Kakao kupitia Mfumo wa kidijitali wa Soko la Bidhaa (TMX) na wakulima walikubali kuuza mazao yao kwa Bei ya Shilingi 25,160 kwa kilo.