Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, amevitaka Vyama vya Ushirika nchini kuwa na Ushirika unaojibu mahitaji ya wananchi kiuchumi na kijamii.

Hayo yamebainishwa  wakati wa Kilele cha Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoani Dodoma lililofanyika kuanzia  Mei 15 hadi 16, 2025 Jijini Dodoma lenye kauli mbiu ya “Ushirika Hujenga Ulimwengu ulio Bora”.

Mheshimiwa Mavunde amesema Ushirika ni Chombo ambacho kinagusa jamii moja kwa moja hivyo ni vizuri vyama vikibuni mambo ya kufanya ambayo yanatatua changamoto na kujibu mahitaji ya Wananchi kiuchumi.

“Niwapongeze sana Vyama vya Ushirika, mnafanya kazi kubwa mnafanya mambo yanayoonekana msibwete sasa fanyeni mambo makubwa na mazuri zaidi ili muweze kunyanyua wananchi kiuchumi; mfanye mambo hayo kwa kuzingatia miongozo ili ushirika uzidi kuleta tija,” amesema Mhe. Mavunde.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Ibrahim Sumbe ameeleza kuwa lengo la jukwaa ni kuwakutanisha Wanaushirika pamoja, ambapo hujadili na kubadilishana uzoefu juu ya fursa zilizopo, mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuzitatua kwa pamoja.

Naye Naibu Mrajis - Uhamasishaji, Consolata Kiluma, amevitaka Vyama viendelee kujiimarisha na kufanya kazi ya kuwahudumia wanachama wao kwa kuzingatia Sheria na miongozo inayotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Aidha, Naibu Mrajis amesema Vyama vinapaswa kuendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kuwahudumia wanachama kwa uharaka, ufanisi na usahihi na hivyo kupunguza manung’uniko miongoni mwa wanachama na kuhakikisha wanaendelea kutumia mfumo wa MUVU na kuingiza taarifa zinazohitajika.