WAZAZI  SEKONDARI NYAISHOZI WATAKIWA KUSIMAMIA MAADILI YA WATOTO WAO  

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt Benson Ndiege ametoa  rai kwa wazazi wa wahitimu wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Nyaishozi kuhakikisha watoto wao wanaporudi nyumbani wanajifunza kazi za mikono ikiwa ni katika kuwajenga na kuwatengenezea njia ya kujiajiri watakapohitimu masomo yao.  

Amesema hayo tarehe 18/04/2024 wakati wa mahafali   ya 12 ya shule ya Sekondari Nyaishozi  inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe (KDCU) iliyoanzishwa mwaka 1990 mkoani Kagera.  

Vilevile amewataka wazazi kuendelea kuwalea wahitimu hao  katika maadili mazuri ili kuendeleza maadili waliyojengewa na walimu wao kwa kipindi cha miaka miwili waliyokuwa shule.

 “Tunawaambia watoto wetu waliomaliza vyuo vikuu wajiajiri ilihali hawajui kufanya kazi za mikono, sasa tumalize hilo tatizo tuwaandae watoto hawa kujiajiri baadae tuhakikishe kazi zote za mikono  wanazijua na wanazifanya kwa kuwaandalia mazingira mapema, hilo ni jukumu letu sote,”  Dkt Ndiege amesema.  

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyaishozi, Audax Gereon, ameushukuru uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe kwa kuona umuhimu wa kujenga shule hiyo ambayo leo hii imewasaidia kupata ajira kwa watumishi wanawake na wanaume 40 na kuomba kuendelea kuilea shule hiyo.  

Naye Mhitimu Lilian Lauriani kwa niaba ya wahitimu aliomba kwa Mgeni rasmi kuwezesha shule ya sekondari Nyaishozi iwe na uhusiano na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ili kuwepo na ufadhili kwa wanafunzi wanaohitimu Nyaishozi sekondari ili waandaliwe chuoni hapo na baadae waweze kuutumikia Ushirika Tanzania nzima kutokana na elimu ya ushirika watakayoipata katika ngazi zote chuoni hapo.  

Wakati huo huo Mrajis Dkt Ndiege alizindua Madarasa  mawili na Mabweni mawili  ya wavulana na kuweka jiwe la mzingi kwa uzio wa shule hiyo.