Wasimamizi wa Vyama vya Ushirika Kanda ya Kaskazini wamepatiwa mafunzo ya mfumo mpya wa kieletroniki utakaosaidia kutunza nyaraka na kumbukumbu za kifedha na mali za Ushirika nchini na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Akizungumza leo tarehe 12/10/2022 wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tatu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwenye ukumbi wa Pius Msekwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Katibu Tawala mkoa huo, William Machum, amesema uhifadhi duni wa nyaraka na kumbukumbu za vyama husababisha kwa baadhi ya vyama kupata hati chafu za ukaguzi.

"Uwazi na uwajibikaji katika kutunza taarifa za fedha na kutokuwepo na mfumo thabithi wa ufuatiliaji wa ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika  nchini huchangia kwa kiasi kubwa vyama hivyo kupata hati chafu na vingine kufa," amesema.

Amesema kuwa mfumo huo utasaidia kuboresha kasi ya ukuaji wa vyama vya ushirika na kudhibiti ubadhilifu wa mali za ushirika na utasaidia kuongezeka kwa uwazi katika utendaji kazi wa vyama.

Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uanzishwaji na uendelezaji wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha vyama vinakidhi matakwa na matarajio ya wanachama na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Naye Mhasibu Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Valency Karunde amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Maafisa Ushirika kutoka kanda ya Kaskazini pamoja Warajis wasaidizi wa vyama vya ushirika wa mikoa hiyo.

"Kupitia mifumo hii itasaidi katika utendaji kazi na ukweli na uwazi wa uendeshaji wa shughuli za vyama na itakuwa rahisi wajumbe kujua kinachoendelea kwasababu kinafanyika kwenye mifumo," amesema Karunde.

Mafunzo hayo pia yanalenga usajili wa vyama ushirika kwa njia za kieletrokini, na yatafanyika kwa siku tatu na inatarajiwa kuwa baada ya mafunzo washiriki watakuwa na uelewa mzuri wa mifumo hiyo.

MWISHO