Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Usamamizi wa Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu amewataka wasimamizi wa maghala kuhakikisha wanafuata sheria na utaratibu wa uendeshaji wa maghala hayo.
Ametoa Kauli hiyo Leo tarehe 14/11/2022 alipokuwa katika ziara ya kikazi iliyowahusisha pia Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho katika Mikoa ya Pwani na Lindi.
Bwana Bangu amesema anataka kusimamia na kufanya kazi na waendesha maghala waaminifu na wanaofuata sheria na hahitaji kufanya kazi na watu ambao hawataki kusimamia misingi na taratibu za kazi zao.
“Tukikubaini unakiuka taratibu na maagizo yetu hatutosita kukufutia leseni yako nafanya hii ziara naangalia yale tuliyokubaliana mnatimiza na kama unajijua hautimizi jitathimini kwasababu sitokuacha salama,” amesema Bangu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) kuweka alama wanazopewa katika vifungashio zinazotambulisha AMCOS hizo.
Amesema kuwa magunia yakiwa na alama itasaidia kupunguza mianya ya udanganyifu ya kuweka vitu katika magunia, hali ambayo inashusha ubora wa Korosho na inaleta picha mbaya kwa wanunuzi.
“Najua sasa hivi udanganyifu umepungua kwa kiasi kikubwa na sasa lengo ni
kumaliza kabisa hali hii, hivyo tunaenda kusajili kila mkulima na kumpa namba yake ambayo itakuwa inabandikwa katika mzigo wake anaopeleka katika AMCOS," amesema Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho.
Pia alisema Mpaka sasa katika makusanyo yanayaofanyika, unyaufu umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na elimu iliyotolewa kwa wakulima ya namna ya kupambana na suala la unyaufu.
Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewaagiza Warajis wa Mikoa na Maafisa Ushirika kutembelea maeneo yao baada ya msimu kuisha ili kukusanya changamoto zilizotokea na kuzitatua ili msimu unaofuata changamoto hizo zisijirudie.
Pia amewataka wataalamu hao kuongea mara kwa mara na wakulima na kuwaambia hali ya soko na bei katika Soko la Dunia kabla ya kuanza kwa minada ili kuepusha sintofahamu zinazojitokeza kipindi cha minada.