Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ametoa rai kwa wakulima nchini kuendelea kujiunga na Vyama vya Ushirika ili waweze kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Ushirika.

Ametoa kauli hiyo tarehe 21/02/2024 wakati wa ziara ya kikazi Wilayani Serengeti alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda (GHOMACOS) na Chama cha Ushirika cha Msingi cha Mazao na Masoko Ngarawani AMCOS.

“Wanachama wa Vyama hivi ni wachache na tunajua Serengeti wakulima ni wengi mjitahidi kujiunga na vyama kwani mnakosa fursa ya masoko na upatikanaji wa pembejeo katika maeneo yenu,” Dkt. Ndiege amesema.

Mrajis ameeleza kuwa amefurahishwa na kasi ya Ushirika unavyoendelea kukua Mkoani Mara na kueleza anaamini nguvu ya Ushirika ya miaka ya nyuma Mkoani humo itarudi tena kwa kasi na kubainisha ulikuwa ni Mkoa ambao Ushirika ulikuwa na nguvu kubwa sana.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha GHOMACOS, Masumbuko Mambasa amesema kupitia Ushirika Chama chao kimeweza kupata soko la pamoja na kuwa na sauti ya pamoja ambayo inawasaidia kuendesha mambo ya Chama kwa urahisi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Uwanja wa Ndege, Joseph Matoke ambaye pia Mwanachama wa Chama cha Ngarawani AMCOS ameomba kuongezewa wanunuzi wa zao la Tumbaku ili kuweza kuwa na ushindani wa bei ambao utawanufaisha wanaushirika wote kwa pamoja.