Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wakulima wakiwemo Wanaushirika hapa nchini kutembelea Taasisi za kifedha kuweza kupata mitaji itakayoweza kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji na kupelekea kujikwamua kiuchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Agosti 01, 2024 alipokuwa akifungua Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.
"Wakulima msiwe na mashaka na mitaji, nendeni Benki mkapate mikopo ya masharti na riba nafuu, nendeni CRDB, NMB, NBC, MKOMBOZI na Taasisisi zingine za kibenki, ukitaka kupata mtaji leo nenda benki, kila benki ina Afisa mmoja wa kuhudumia Wakulima na hii ni pamoja na wanaushirika nendeni benki mkapate mkopo" amesema Waziri Mkuu
Aidha, Waziri Mkuu amezitaka Sekta mbalimbali hapa nchini hususan Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika kuimarisha Sekta hizo na kutumia teknolojia ya kisasa .
Waziri Mkuu amesema maonesho haya yanalenga kutoa fursa kwa Wakulima, Wafugaji, Wanaushirika, wajasiriamali na wasindikaji, kujifunza teknolojia mbalimbali kutoka kwa wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Sekta binafsi na wataalamu walioko Serikalini, kuonyesha umuhimu wa Sekta hizo inavyoleta tija kwenye maisha ya kila mtu katika siku zote za maisha yake.
Maonesho haya ya Kimataifa ya Wakulima yameanza leo Agosti 01, 2024 na kilele chake kitakuwa Agosti 08, 2024.