Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika (Masoko na Uwekezaji), Revocatus Nyagilo ametembelea Mabanda ya Vyama vya Ushirika yaliyopo katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara maarufu SABASABA leo Julai 07, 2023 kwenye viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Ametoa rai kwa Vyama vya Ushirika kuchangamkia fursa za kimasoko zinazopatikana kutoka mataifa mbalimbali na kuhakikisha wanaochakata mazao yanayozalishwa ili kupata bidhaa zitakazokidhi ushindani wa soko huria.

Aidha,  ameshauri Vyama kuajiri wataalam wenye uzoefu wa kutafuta masoko ya mazao na bidhaa za Vyama pamoja na kutafuta taarifa za masoko na kufahamu washindani katika soko la ushindani.

Vilevile amesema Viongozi wa Vyama waache kufanya kazi kwa mazoea bali kwa kufuata misingi, taratibu na Sheria ya Vyama vya Ushirika na viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha wanachama wao hawauzi Mazao yao kwa mfumo usio rasmi kwani huchangia uchumi wa Vyama kuyumba na kudhoofisha Maendeleo ya Vyama hivyo.

Amesema kuuza kwa mazao kwa mifumo isiyo rasmi ni kumkosesha Mkulima haki anayostahiki kuipata hivyo ni wajibu wa viongozi kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wao juu ya umuhimu wa kuuza mazao yao kwa taratibu za kiushirika kwa kufuata mifumo iliyowekwa.

Mrajis Msaidizi ametembelea Banda la WETCU 2018 LTD, KYECU LTD, RUNALI LTD, AWIB SACCOS LTD, DASICO LTD, SHIRECU LTD na KDCU LTD.