Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameeleza kuwa,   ili Ushirika uzidi kusimama na kukua vizuri ni lazima matumizi ya mifumo ya kidigitali itumike katika shughuli za kila siku za chama ambapo itazidi kuonesha na kusimamia uwazi katika Vyama hivyo.

Hayo yameelezwa tarehe 02/03/2024 katika kikao baina  ya Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa  TCDC, Mkurugenzi Mkuu COPRA , Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) , Mkurugenzi  wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) pamoja na Viongozi wa Vyama Vikuu vya RUNALI, TANECU na MAMCU.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Madeje, ameeleza kuwa mfumo wa kidigitali utatumika wakati wa minada na hauji kubadili mambo mazuri yanayofanyika kipindi hiki kama vile wakulima kulipwa fedha za mazao waliyouza kwa wakati.

“Huu mfumo unakuja kuboresha uwazi na kuongeza ufanisi na utakuwa unaendeshwa na Vyama vyenyewe kwasababu wao ndiyo wenye wakulima na ndiyo wanaofanya kazi moja kwa moja  na wakulima katika maeneo yao pia utaongeza wigo wa wanunuzi katika minada,” amesema Mandeje

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzyi, ameeleza ili mfumo huo uweze kupokelewa vizuri na kutumika ipasavyo ni vyema Wataalamu wa TMX, COPRA na TCDC waende kuweka kambi na kutoa elimu zaidi kwa watumiaji ili uweze kutumika na kufikia malengo yanayotarajiwa.