Kaimu Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Emmanuel Lema, amatoa rai kwa Viongozi wa Vyama vya ushirika kuhakikisha wanachama wao wanamaliza hisa ili kuhakikisha Vyama vinakuwa imara na endelevu.

Ameeleza Chama ni mali ya Wanachama wenyewe hivyo ni lazima kila mwanachama ahakikishe anamalizia hisa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2023 na Masharti ya Chama ili kuweza kujenga mtaji wa ndani wa chama na kuwa imara kiuchumi.

Ameeleza hayo leo tarehe 12/06/2024 wakati akifunga mafunzo yaliyoratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ya Wajumbe wa Vyama vya Ushirika vya Mbogamboga yaliyofanyika Mkoani Kilimanjaro.

Aidha, amewataka Viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza Vyama hivyo kutambua kuwa Vyama vya ushirika si mahala pa kuchuma mali na kuondoka; Ushirika wa sasa hauna nafasi ya kufanya ubadhilifu.

“Naendelea kuwasihi Viongozi wa Bodi waendelee kuwahamasisha Wananchi ikiwemo Vijana na Wanawake kuendelea kujiunga na Vyama vya Ushirika vilivyopo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji, kuhimili ushindani na uchumi imara wa Vyama,” amesema Dkt. Lema.

Vilevile amewataka Washiriki wa Mafunzo haya kutekeleza walichojifunza kwa vitendo na kuhakikisha Wanachama wanaendeleza kilimo cha Mazao ya Bustani kwa Maendeleo yao wenyewe na kwa jamii inayowazunguka.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wajumbe wa Bodi, Abduel Yairo, amesema mafunzo waliyoyapata wataenda kuyafanyia kazi na kuwarudishia mrejesho wanachama wengine ili kuendelea kuwa na chama bora na imara.

"Tunahitaji kuwezeshwa zaidi kwa mafunzo mengine ili kuongeza ujuzi na uelewa zaidi kuweza kutekeleza majukumu yetu kama viongozi wa Bodi zetu kwa niaba ya wanachama wote," amesema Yairo.