Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Jacqueline Senzighe, amewataka Viongozi wa bodi za Vyama vya Ushirika wa Mbogamboga kutambua wajibu wao katika Vyama na kutowaachia watendaji kuendesha Vyama hivyo.

Ameeleza kuwa Chama ni cha wanachama na si cha watendaji hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanakisimamia chama chao katika shughuli zote za utendaji.

 "Ili kiwe chama bora ni lazima Viongozi wazingatie maadili ya uongozi kwani kiongozi ndiyo muonesha njia na kiongozi ndiyo anaweza kujenga au kubomoa chama chake akiwa hatokuwa na maadili," amesema Jacqueline.

Ameeleza hayo Leo tarehe 10/06/2024 wakati akifungua mafunzo yaliyoratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ya Wajumbe wa Vyama vya Ushirika vya Mbogamboga yaliyofanyika Mkoani humo.

Aidha, Mrajis Msaidizi amewataka viongozi hao kuzingatia Sheria zote za uendeshaji wa vyama watakazofundishwa ambazo ndiyo miongozo ya uendeshaji wa Vyama.

“Tume haijawaacha wakiwa, hivyo msiwe na hofu ya mtaendeshaje Vyama vyenu niwatoe wasiwasi, TCDC imetoa miongozo ambayo itawaongoza na ni vyema ikafuatwa ili mjenge hivyo vyama viwe imara,” amesema.

Naye Mrajis Msaidizi  wa (Uhamasishaji), Ibrahim Kadudu, ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni  kuwanjengea uwezo Viongozi wa Vyama hi yo ili kuelewa kiundani dhana za Ushirika na kujua Vyama vya Mbogamboga vinaendeshwaje.

Mafunzo hayo yamehusisha taasisi mbalimbali  ikiwemo Wizara ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCu), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI).