Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Kilimo kuiangalia kwa jicho la kipekee Sekta ya Ushirika ili kujenga Vyama vya Ushirika vilivyo imara ili kurejesha hadhi na mchango wa Ushirika hapa nchini.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Agosti 08, 2024 alipokuwa akifunga Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
"Ili mageuzi makubwa tunayoyafanya kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi yalete matokeo ya uchumi endelevu ni lazima tujenge Vyama vya Ushirika vilivyo imara; hivyo Wizara ya Kilimo naitaka itupie jicho kwenye Sekta hii ili kurejesha hadhi na mchango wa Ushirika nchini," amesema Mhe. Rais.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka Wakulima kutokuwa na hofu na mitaji kwakuwa Serikali inakwenda kuongeza upatikanaji wa Mikopo kwa riba nafuu kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.
Kwa upande mwingine Rais Dkt. Samia amewahakikishia Wakulima upatikanaji wa Masoko na kutoa ruzuku ya mbegu kwa Wakulima na kuwataka kujisajili kwenye mfumo ili kunufaika kwa ruzuku hizo. "Lengo la Serikali ni kuwasaidia wakulima, ili waweze kujitegemea," amesema Mhe.Rais Dkt. Samia.