Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi amezitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) na Muungano wa Vyama vya Ushirika (SCCULT) kuhakikisha kuwa wanatengeneza Mifumo, Taratibu na Kanuni imara ili kuendeleza Vyama Ushirika vilivyo imara.

Ametoa rai hiyo leo Januari 10, 2025 katika kikao kazi cha kujadili mwelekeo wa Serikali kuhusu Maendeleo ya Ushirika nchini kilichowashirikisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) na Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) kilichofanyika Jijini Dodoma.

"Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kuhakikisha inasimamia vyema Vyama vya Ushirika ila jambo la muhimu serikali inalolitaka kwenu TCDC, TFC na SCCULT, tengenezeni Mifumo, taratibu na Kanuni imara ili kuendeleza Vyama na kuwa na Ushirika imara na wenye nguvu," amesema Dkt. Nindi.

Aidha, ameongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na utitiri wa Vyama vya Ushirika ambavyo havisaidii katika kukuza Sekta ya Ushirika ni bora kuwa na Vyama vichache ambavyo vitasimama imara na kuweza kuwatetea Wanachama hasa Wakulima ambao ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya kibiashara na hivyo kuimarisha Sekta ya Kilimo hapa nchini.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ushirika, Irene Madeje, amesema kuwa ili kujenga taswira ya Ushirika iliyosimama kibiashara na Ushirika imara na wenye nguvu ni lazima Vyama vizingatie maelekezo ya Serikali na kutekeleza Vipaumbele vinane vya Ushirika vilivyotolewa na Kamisheni na Wanaushirika.

Akivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni, Uwekezaji katika Mifumo ya kisasa ya kidigitali, Kuimarisha Maendeleo ya Benki ya Ushirika, Kuhamsisha Mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara, Kuboresha Sera, Sheria na Usimamizi wa Ushirika, Kuhamasisha Ushirika kwenye Sekta mbalimbali na Makundi maalumu, Kuimarisha Uwekezaji na Mali za Ushirika katika uzalishaji, kushirikiana na Wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zilizopo kwenye Ushirika na Kuboresha maslahi ya Watumishi na Mazingira ya Utendaji kazi.

Kwa upande wake, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, ametoa rai kwa Bodi za TFC na SCCULT kuhakikisha kuwa Ushirika unamnufaisha kwanza Mwanaushirika mwenyewe na si vinginevyo na kusisitiza Ushirikiano baina ya TCDC na Bodi hizi ili kuweza kutoka hatua moja na kwenda hatua nyingine katika kuendeleza Vyama vya Ushirika.

"Nitoe wito kwenu TFC, SCCULT na Vyama vya Ushirika kuhakikisha mnashirikiana Vema na TCDC ili kuhakikisha yale mazuri tunayoyafanya katika katika Vyama vyetu yanatangazwa na hivyo kuleta mwamko na kuhamasisha Wananchi wengi zaidi wanafahamu mazuri ya Sekta ya Ushirika na si vinginevyo," ameyasema Dkt. Ndiege.

Wakitoa taarifa ya Maendeleo ya taasisi zao, Mwenyekiti wa TFC, Tito Haule na Mwenyekiti wa SCCULT, Ernest Nyambo, wamepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na TCDC katika kuhakikisha Ushirika unasimama imara. Aidha, wamewataka Viongozi wa Bodi za Vyama vya Ushirika kuwa waadilifu na waaminifu katika kusimamia Vyama kwaniaba ya wanachama.