Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC),Bodi ya Stakabadhi za Ghala(WRRB) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) wamesaini Randama ya Makubaliano (MoU) na CRDB FOUNDATION kwa ajili ya kuviwezesha  Vyama vya Ushirika kupata mikopo nafuu kupitia 'product' ya "imbeju".

Makubaliano hayo  yametiwa saini leo tarehe 16/02/2024 Jijini Dar es salaam ambapo Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa Tume katika kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinajiendesha kibiashara ikiwemo kuwa na mitaji kupitia mikopo ya gharama nafuu imeanzisha mahusiano na CRDB Foundation.

"Katika kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinajiendesha kibiashara ikiwemo kuwa na mitaji kupitia mikopo ya gharama nafuu pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika zikiwemo kuendelea na uanzishwaji wa Benki ya Ushirika,Tume imeanzisha mahusiano  na CRDB Foundation ili kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinapata mikopo nafuu," amesema Dkt. Ndiege.

Akitaja malengo ya Makubaliano hayo Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tuli Esther Mwambapa, amesema malengo hayo ni pamoja na kuvikopesha Vyama vya Ushirika mizani ya kidigitali pamoja na viambata vyake (vishikwambi, kompyuta na POS), Kuwajengea uwezo watendaji, Viongozi wa Vyama na Wanachama wa Vyama vya Ushirika juu ya Matumizi ya Huduma za kifedha ( Capacity Building and Financial Literacy Training), kuwezesha maghala ya kuhifadhi mazao kuwa na teknolojia ya kisasa katika usimamizi wake na kuboresha Mifumo ya Usimamizi wa Masoko kwa TMX.