Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume itaendelea kuwajengea uwezo Watumishi katika utendaji na utekelezaji wa Majukumu yao ili kuongeza Ufanisi wa kazi kwa lengo la kuimarisha Sekta ya Ushirika.
Amesema hayo wakati akitoa Taarifa yake kwa Watumishi wa Tume wakati wa Kikao cha Watumishi Wote wa Tume Makao Makuu na Mikoani kilichofanyika Desemba 18, 2024 Jijini Dodoma.
Amebainisha kuwa Tume hufanya Vikao vya watumishi wote kila mwaka kwa lengo la kujadili kwa pamoja fursa na namna bora ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika utendaji.
Amesema Tume tayari imekuwa na utaratibu wa kupeleka Watumishi wake katika Mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika Ngazi mbalimbali za masomo na kutenga fedha pamoja na Mpango wa mafunzo kwa Watumishi.
“Nitoe rai kwa Watumishi kutumia fursa za kujiendeleza hasa kitaaluma ili kujiongezea maarifa mapya kwaajili ya kujenga Ushirika imara,” amesisitiza Mrajis.
Aidha, amesisitiza matumizi ya Mifumo ya TEHAMA ya kiutendaji kama vile Mfumo wa Upimaji wa Utendaji (e- Utendaji) ambao husaidia katika kufanya tathmini ya utendaji wa majukumu ya Watumishi na Taasisi kwa ujumla, jambo linalosaidia kujua hali ya utendaji wa Taasisi ili kujua namna bora ya kuongoza na kusimamia huduma Bora za Ushirika.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo, Agnes Hugo, ameipongeza Tume kwa jitihada za kuendeleza na kujali Maslahi ya Watumishi kwa kuzingatia masuala yenye kuongeza Motisha na morali ya Kazi kwa Watumishi wa Tume.
Watumishi wa Tume wameishukuru Tume kwa kuendelea kuboresha Mazingira ya Kazi na maslahi ikiwemo Mafunzo ya kuwajengea Uwezo, Michezo, maboresho ya Muundo pamoja na masuala ya Kijamii.
Kikao hicho kimejumuisha Watumishi wote katika Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa njia ya Mtandao.