Naibu Waziri wa Kilimo wa Kilimo, Mhe. David Silinde, ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuendendelea kusajili Vyama vingi vya Ushirika kwakuwa Ushirika ndio njia pekee ya kuwasaidia wakulima kuweza kuondokana na changamoto za Masoko.
Naibu Waziri ametoa rai hiyo Oktoba 08, 2024 wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo ya awamu ya tatu yaliyofanyika katika Viwanja vya shule ya Msingi Gairo Wilayani Gairo Mkoani Morogoro.
"kupitia maonesho haya naiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kusajili Vyama vingi vya Ushirika, kwakuwa Ushirika ndio njia pekee ya kumsaidia mkulima kutatua changamoto za masoko pamoja na upatikanaji wa pembejeo za Kilimo," amesema Mhe. Silinde.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa Gairo na wananchi wote nchini kuendelea kujiunga na Vyama vya Ushirika na kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwasababu ndio mkombozi wao katika Sekta ya Kilimo.
Hali kadhalika amewasisitiza Wakulima kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi ghalani kwa kutumia Mfumo wa Soka la Bidhaa Tanzania (TMX) ili kupata bei za ushindani kwa mazao yao na hivyo kuongeza kipato chao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Jabiri Makame, amesema lengo la Maonesho hayo ni kuwafikia Wakulima wa chini wa ngazi ya Kata na Vijiji ambao wengi wao hushindwa kusafiri kwenda Morogoro mjini kuhudhuria Maonesho Wakulima ya ngazi ya Mkoa Maarufu kama Nanenane.
"Kwa kutambua hilo tulianza kufanya maonesho hayo ambayo yameonyesha kuleta matokeo chanya kwa wakulima kubadili mfumo wa Mazoea na kulima kilimo cha Kisasa," amesema Mhe. Makame.
Kwa upande wake Naibu Mrajis (Uhamasishaji), Consolata Kiluma, amesitiza matumizi ya Mifumo ya kidigitali ya Ununuzi kupitia Vyama vya Ushirika, Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Mfumo wa Stakabadhi za ghala ( WRRB) ili wananchi waweze kuwa na uwazi na uhakika wa bei ya mazao yao.